Israel Yapiga Marufuku Drones Zote za Kiraia kwa Miezi 6 Kumlinda Netanyahu 🚁
Israel imeripotiwa kuweka marufuku ya miezi sita kwa matumizi ya ndege nyuki (drones) za kiraia. Uamuzi huu wa dharura unakuja kutokana na hofu kubwa ya kiusalama kwamba vyombo hivyo vinaweza kutumiwa na maadui kufanya mashambulizi dhidi ya viongozi waandamizi wa serikali na jeshi.
Mamlaka za Israel zinahofia kuwa Iran au makundi yanayoungwa mkono na Iran, yanaweza kutumia drones za kawaida za kibiashara kufanya mauaji ya kulenga viongozi wakuu, akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Zuio hili linalenga kupunguza hatari ya drones hizi kubadilishwa mfumo (modified) na kutumika kwa ujasusi au kushambulia maeneo nyeti na watu wanaolindwa sana.
Hili ni moja ya vizuizi vikubwa zaidi kuwahi kuwekwa na Israel hivi karibuni, likionyesha jinsi vyombo hivi vinavyoendeshwa bila rubani vilivyobadilisha kabisa mbinu za kivita.
Serikali bado haijatoa ufafanuzi wa kina wa kisheria kuhusu utekelezaji wa marufuku hii, lakini taharuki ni kubwa.
Zamani, kufanya shambulio dhidi ya kiongozi mkuu wa taifa kulihitaji ndege za kivita au makombora yenye thamani ya mabilioni ya dola. Leo, drone ya kibiashara inayonunuliwa mtandaoni kwa dola 1,000 inaweza kufungwa vilipuzi (C4) na kuleta madhara makubwa. Israel ina mifumo imara zaidi duniani ya ulinzi wa anga (Kama Iron Dome), lakini mifumo hii imeundwa kudungua makombora makubwa yanayoruka juu, sio drones ndogo za plastiki zinazoruka chini chini (low altitude).
Sio lazima drone ibebe bomu ili iwe hatari. Hofu nyingine ya Israel ni ujasusi. Makundi ya wapiganaji yanaweza kutumia drones za kiraia kurekodi mienendo ya misafara ya viongozi, ramani za makazi yao, na udhaifu wa ulinzi wao, kisha kutuma taarifa hizo Tehran au Beirut kwa ajili ya kupanga mashambulizi kamili.
Swahili Prime Ent
Comments
Post a Comment